Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, mwaka mmoja umepita tangu kuanguka serikali ya awali ya Syria iliyokuwa na taswira ya kiusalama na kijasusi; mfumo ambao nafasi yake ilichukuliwa na serikali mpya yenye watu na nyuso zilizowatia moyo wananchi wa Syria kwa ahadi za uhuru na kwa kuzikosoa sera za kiusalama za serikali iliyopita. Hata hivyo, haijachukua muda mrefu kabla ya serikali mpya kuziacha ahadi hizo, na magereza yamejaa tena wafungwa.
Shirika la habari la Reuters, katika ripoti yake, lilibainisha kuwa magereza na vituo vya mahabusu vimejaa tena maelfu ya watu waliokamatwa; hali ambayo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu.
Katika uchunguzi uliotajwa kwenye ripoti ya shirika hilo la habari, imeelezwa kuwa baadhi ya magereza yaliyokuwa yamefungwa baada ya kuanguka kwa serikali ya awali, yameanza tena shughuli zake katika kipindi cha mwaka uliopita, licha ya ahadi za rais wa serikali ya mpito, Abu Muhammad al-Joulani, anayejulikana kama al-Shar‘a, za kufunga magereza yenye sifa mbaya na kufunga kabisa faili za kukamatwa kiholela; ahadi ambayo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, hali halisi inaonesha kuwa haikutekelezwa kikamilifu.
Mandhari ya kukamatwa tena kwa nguvu imerejea na kuwa sehemu ya uhalisia wa Syria ya baada ya vita. Mawimbi ya kamata kamata yamewakumba Wasyria wanaotikana na asili na makundi mbalimbali; visingizio vinatangazwa kuwa ni kulinda usalama, na mashtaka yako tayari.
Licha ya tofauti ya muktadha wa kisiasa kati ya mfumo wa awali na mfumo wa sasa, matokeo ni yale yale: msongamano katika vituo vya mahabusu, kushikiliwa bila kufunguliwa mashtaka ya wazi, na kukosekana kwa njia za kisheria zilizo wazi na zenye uwazi.
Serikali ya Damascus, ikijaribu kuhalalisha hali ya kiusalama inayofanana na ya zamani, inasema kuwa ukamataji unafanyika katika muktadha wa kuwafuatilia wale waliokuwa wamehusika katika uhalifu na makosa, na kwamba nchi ipo katika hatua ya mpito inayohitaji kujengwa upya kwa taasisi za kiusalama na za mahakama.
Hata hivyo, watetezi wa haki za binadamu wanatahadharisha kuwa; kuendelea kwa ukamataji wa makundi makubwa ya watu na ukosefu wa uwazi, kunadhihirisha tena hali ya hofu na kunayumbisha imani kutokana na ahadi zilizotolewa sambamba na hatua mpya.
Na katikati ya ahadi za mageuzi na uhalisia wa magereza yaliyojaa wafungwa, faili la waliokamatwa linabaki kuwa mtihani wa hatima kwa uwezo wa Syria mpya kujenga dola inayotawaliwa na sheria; dola ambayo ndani yake, vizimba vya magereza havitakuwa tena alama ya utawala.
Maoni yako